Jumamosi 31 Oktoba 2026 - 07:10
Tujifunze kwa Bibi Zahraa (as) Jinsi ya Kulea Watoto Wachamungu na Wenye Maadili

Hawza/ Sheikh Mkuu wa Jumuiya ya Shia Tanzania (TIC), Maulana Sheikh Hemed Jalala Mwakindenge, ameitaka jamii ya Kiislamu kuweka mkazo katika malezi bora ya watoto kwa kuzingatia misingi ibada na kumcha Mwenyezi Mungu, huku akisisitiza kuwa maisha ya Bibi Fa'timah Zahraa (as) ni mfano bora wa kuigwa katika malezi ya kizazi chenye maadili mema.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, Sheikh Hemedi Jalala, ambaye pia ni Imam Mkuu wa Msikiti wa Ghadir uliopo Kigogo Post, jijini Dar es Salaam, ameyasema hayo katika hotuba yake ya Swala ya Ijumaa iliyoswaliwa jana, ambapo ameeleza umuhimu wa wazazi kujifunza kutoka katika maisha ya Bibi Zahraa (as), hasa namna alivyolea watoto wake katika mazingira yaliyojengwa juu ya imani, uchamungu na kumtii Mwenyezi Mungu (swt).

Mkurugenzi wa Hawza ya Ima'm Swa'diq (as) alianza hotuba yake kwa kusoma aya tatu za Suratul-Kawthar na kusema:

{ إِنَّاۤ أَعۡطَیۡنَـٰكَ ٱلۡكَوۡثَرَ }، { فَصَلِّ لِرَبِّكَ وَٱنۡحَرۡ }، { إِنَّ شَانِئَكَ هُوَ ٱلۡأَبۡتَرُ }.

Hakika Sisi tumekupa Al-Kawthar (kheri nyingi), Basi swali kwa ajili ya Mola wako na uchinje (kwa ajili Yake), Hakika anayekuchukia ndiye atakayekuwa mwenye kukatika (na kila kheri).

(Suratul-Kawthar: 1–3).

Akizifafanua aya hizo, Sheikh Jalala alieleza kuwa: Neno Al-Kawthar lililotajwa katika sura hiyo, kwa mujibu wa baadhi ya tafsiri, linahusishwa na Bibi Fa'timah Zahraa (as). Alitumia ufafanuzi huo kama utangulizi wa mada aliyokusudia kuizungumza, ambayo ni malezi bora ya watoto na umuhimu wa kuwa na mifano halisi ya kuigwa katika kuijenga familia na jamii yenye maadili mema.

Alibainisha kuwa: Kutokana na kipindi hiki kusadifiana na kumbukumbu ya shahada ya Bibi Zahraa (as), ameamua kumfanya mtukufu huyo kuwa kiigizo chema katika kuzungumzia suala la malezi, huku akionesha namna ambavyo maisha yake yanavyoweza kuwa mwongozo kwa wazazi katika kuwalea watoto wao hasa mabinti.

Mwezi wa Jumada al-Ula na kumbukumbu ya matukio ya kihistoria

Katika sehemu nyingine ya hotuba yake, Sheikh Mkuu wa Mashia Tanzania, alizungumzia namna baadhi ya jamii za mwambao wa Afrika Mashariki zinavyouzingatia mwezi wa Jumada al-Ula, unaojulikana pia kama Mfungo Nane, kutokana na kuhusishwa kwake na kumbukumbu ya shahada ya Bibi Zahraa (as).

Alieleza kuwa katika jamii hizo, mwezi huu hushuhudiwa bila kufanyika sherehe mbalimbali, ikiwemo sherehe za harusi, kama ilivyo katika miezi ya Muharram na Safar. Alidokeza kuwa huenda utaratibu huo una uhusiano na matukio mazito yaliyotokea katika historia ya Uislamu, ingawa baadhi ya watu wanaouendeleza utamaduni huo huenda hawana ufahamu wa kutosha kuhusu chimbuko na sababu zake za kihistoria.

Kwa mujibu wa maelezo yake, ni muhimu kwa jamii kuelewa historia inayohusiana na miezi na matukio hayo, ili mila na taratibu zinazotekelezwa ziweze kuambatana na ufahamu sahihi wa misingi yake.

Wito wa kulinda umoja wa Kiislamu licha ya tofauti za kihistoria

Akiendelea na hotuba yake, Sheikh Mkuu wa Mashia Tanzania aligusia wosia wa Shahidi Imam Khamenei, kuhusu namna ya kuzungumzia matukio ya kihistoria yanayohusiana na kipindi hiki, akisisitiza umuhimu wa kuzingatia umoja wa Waislamu wakati wa kueleza historia ya Bibi Zahraa (as). Alisema kuwa mtu anapoisoma historia ya Bibi Zahraa (as) na matatizo aliyokumbana nayo, atabaini kuwa yalikuwa ni matukio makubwa na ya kutisha, yaliyoambatana na dhulma za wazi na vitendo vya kikatili.

Hata hivyo, alisisitiza kuwa pamoja na uzito wa matukio hayo ya kihistoria, Waislamu wanapaswa kuwa waangalifu katika kuchagua maneno wanayotumia wanapoyazungumzia, hususan katika hotuba na mikusanyiko ya kidini, ili maelezo yao yasiwe chanzo cha mifarakano na migawanyiko katika jamii.

Aliongeza kuwa: Bila kujali tofauti zilizopo katika mitazamo ya kihistoria, ni wajibu wa Waislamu kulinda tunu muhimu ya umoja wa Kiislamu na kuiepuka migogoro inayoweza kudhoofisha mshikamano wao.

Uchamungu: Msingi mkuu wa malezi ya Bibi Zahraa (as)

Akirejea katika mada kuu ya hotuba yake, Sheikh Hemedi Mwakindenge, alieleza kuwa: Msingi mkubwa wa malezi na mwenendo wa maisha ya Bibi Zahraa (as) ulikuwa ni ibada na kumcha Mwenyezi Mungu (swt). Alibainisha kuwa nafasi kubwa ya ibada katika maisha ya mtukufu huyo inadhihirishwa pia kupitia zawadi maalumu ya Tasbihi ya Bibi Zahraa (as) aliyoipata kutoka kwa baba yake, ambayo imeendelea kuwa miongoni mwa dhikri zinazotiliwa mkazo katika mafundisho ya Kiislamu.

Aidha, alieleza kuwa nyumba ya Bibi Zahraa (as) ilikuwa ni nyumba iliyojengwa juu ya misingi ya ibada, dua, kumdhukuru Mwenyezi Mungu na kumtii Yeye. Mazingira hayo ya kiroho na kimalezi yalikuwa na nafasi kubwa katika kuandaa kizazi chenye sifa na utukufu wa hali ya juu.

Alifafanua kuwa: Katika nyumba hiyo ndipo walipolelewa na kukua watu watatu miongoni mwa shakhsia kubwa katika historia ya Uislamu, ambao ni Imam Hassan (as), Imam Hussein (as) na Bibi Zainab (as).

Kwa msingi huo, Mkurugenzi wa Hawza ya Imaam Swa'diq (as), alisisitiza kuwa: Mafanikio ya malezi hayawezi kutenganishwa na mazingira ya kiroho na kimaadili yanayojengwa ndani ya familia. Hivyo, wazazi wanaotamani kuona watoto wao wanakuwa watu wenye imani, maadili na mwenendo mwema wanapaswa kuanza kwa kujenga mazingira ya uchamungu ndani ya nyumba zao.

Alimalizia hotuba yake kwa kusisitiza kuwa: Bibi Zahraa (as) ni mfano bora wa kuigwa katika malezi ya watoto, kwani katika maisha yake yote hakuna jambo alilolipa nafasi ya kwanza zaidi ya kumcha Mwenyezi Mungu (swt). Hivyo, jamii inapaswa kujifunza kutoka katika mwenendo wake na kuufanya kuwa msingi wa malezi ya kizazi kijacho.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha